Saturday, May 9, 2015

Kifaa cha Pluijm Yanga SC

Na Wilbert Molandi
Dar es Salaam
KOCHA wa Yanga, Hans van Der Pluijm, amewatoa hofu mashabiki na wanachama wa timu yake kwamba atasajili winga hatari kuziba pengo la Mrisho Ngassa anayetimkia Free State Stars ya Afrika Kusini.
Ngassa ambaye mkataba wake umeisha siku chache zilizopita, muda mrefu alikuwa ameshasaini kuichezea timu hiyo ya Afrika Kusini na alibaki nchini kumalizia muda wa kuitumikia Yanga. Championi lilikuwa gazeti la kwanza nchini kuandika habari ya Ngassa kusajiliwa na Free State Aprili 4, mwaka huu.
Pluijm, raia wa Uholanzi, aliliambia Championi Jumamosi kuwa, mashabiki wasiwe na hofu kuhusu kuondoka kwa Ngassa kwani hakuna ubaya wowote kwa mchezaji kuondoka, isipokuwa wanatakiwa kumuombea maisha mema aendako.
“Sina hofu yoyote kuhusu kuondoka kwa Ngassa, japokuwa ni mchezaji mwenye uwezo mzuri na unayeweza kumtegemea kikosini, lakini hakuna jinsi, ni lazima aondoke, ingekuwa ngumu kumzuia.
“Mashabiki waondoe hofu kwani timu ndiyo inaingia katika kipindi cha usajili ambacho tutasajili mchezaji kama Ngassa uwanjani lakini huyo mpya atakuwa hatari zaidi,” alisema Pluijm.Katika mchezo dhidi ya Azam FC katikati ya wiki hii, Ngassa alitumia muda mwingi kuwaaga mashabiki wa Yanga baada ya mchezo huo ambao Azam ilishinda mabao 2-1.

Okwi: Simba tulieni, tutapanda ndege mwakani

Martha Mboma na Mussa Mateja
SIMBA leo inacheza na JKT Ruvu kukamilisha ratiba ya Ligi Kuu Bara ikiwa imekosa nafasi ya pili, lakini nyota wake Emmanuel Okwi amewapoza mashabiki wa timu hiyo na kuwaahidi mambo makubwa msimu ujao.Akizungumza na Championi Jumamosi, Okwi alisema ana uhakika msimu ujao kikosi chake kitajitahidi na kushika moja kati ya nafasi mbili za juu na kushiriki michuano ya kimataifa.
“Mambo tu hayakwenda kama tulivyotarajia msimu huu, tulijitahidi kadiri ya uwezo wetu ili angalau tupate nafasi ya pili lakini ndiyo kama mlivyoona, wenzetu walikuwa wazuri zaidi.
“Nawaambia tu Wanasimba watulie ili msimu ujao tufanye kazi yetu na tutapata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa,” alisema Okwi, raia wa Uganda. Okwi alisema moja ya sababu za kutofanya vizuri kwa kikosi chao ni kuwa na wachezaji wengi ambao hawakuwa na uzoefu wa Ligi Kuu Bara, pia kutumia mifumo miwili ya makocha katika msimu mmoja ilikuwa tatizo.
Yanga ndiyo iliyotwaa ubingwa wa Bara na itashiriki Ligi ya Mabingwa mwakani na Azam FC imeshika nafasi ya pili na itacheza Kombe la Shirikisho Afrika.

Yanga yamuuza Msuva Sh bilioni moja


Winga wa Yanga, Simon Msuva.
Na Wilbert Molandi
Dar es SalaamWINGA wa Yanga, Simon Msuva anaendelea vizuri na majaribio katika kikosi cha Bidvest Wits ya Afrika Kusini, uongozi wa timu yake umesema kama akifuzu upo tayari kumuuza kwa dau la dola 700,000 (zaidi ya Sh Bilioni 1.3).
Yanga imeamua kukata mzizi wa fitina baada ya Msuva kutoroshwa katikati ya wiki hii kwenda Afrika Kusini kufanya majaribio katika klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu Afrika Kusini (PSL).
Msuva ambaye mkataba wake unafikia tamati msimu ujao, leo anamaliza majaribio na kurejea nchini usiku na kama akifuzu atakuwa ameitajirisha klabu yake ambayo tayari imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara ambapo leo inakamilisha ratiba kwa kucheza na Ndanda FC kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.
Winga huyo aliyesajiliwa na Yanga misimu miwili iliyopita akitokea Moro United, sasa anasubiri tuzo yake ya ufungaji bora kwani hadi sasa amefunga mabao 17 akifuatiwa na Amissi Tambwe aliyefunga 17. Hata hivyo, Tambwe anaweza kuongeza mengine leo katika mchezo dhidi ya Ndanda.
Kama Msuva akifanikiwa katika majaribio yake anaweza kumtoa kikosini Christopher Katongo raia wa Zambia au Fikru Tefera wa Ethiopia ambao wanaichezea timu hiyo inayomilikiwa na Idara ya Michezo ya Chuo Kikuu cha Bidvets maarufu kama Wits.
Katibu Mkuu wa Yanga, Dk. Jonas Tiboroha, alilihakikishia Championi Jumamosi kuwa, kila mchezaji wa kikosi hicho ana thamani yake lakini wenye viwango vya wastani ni dola 500,000 (Sh milioni 965) na wenye uwezo wa juu ni dola 700,000.
Hiyo ina maana, Msuva ambaye yupo katika kundi la wachezaji wenye viwango vya juu kikosini kwa sasa ana thamani ya dola 700,000.
“Hatumzuii mchezaji kwenda kuichezea timu nyingine, lakini lazima klabu inayomuhitaji ifuate utaratibu ili tupate haki zetu, mchezaji mwenye kiwango cha wastani tunamuuza kwa dola 500,000 na yule mwenye kiwango cha juu ni dola 700,000,” alisema Tiboroha.
“Pia tuna kigezo kingine ambacho tutakitazama kwamba ni lazima timu inayomnunua mchezaji wetu iwe inashiriki michuano ya kimataifa, maana fedha si kila kwetu.”
Endapo Msuva atafanikiwa kujiunga na Bidvest, atakuwa mchezaji wa pili wa kutegemewa na Yanga aliyeshiriki kikamilifu kuipa ubingwa msimu huu kuondoka kwani wa kwanza ni Mrisho Ngassa anayetimkia Free State Stars ya Afrika Kusini pia.

Azam: Huyo Kavumbagu aondoke tu

Na Nicodemus Jonas
Dar es SalaamAZAM FC imefikiria kuhusu straika wake, Didier Kavumbagu kutingisha kiberiti na kutaka kurudi Yanga, kisha ikasema wala hakuna shida aende tu.Siku kadhaa nyuma mabosi wa Yanga waliokuwa katika harakati za kumshawishi Kavumbagu arejee kwenye kikosi chao ili kuimarisha safu ya ushambuliaji na Azam ilikuwa kimya tu.
Kaimu Kocha wa Azam, George ‘Best’ Nsimbe ametoa mkono wa baraka kwa mchezaji huyo kuangalia mbele zaidi kwa manufaa yake endapo anadhani Yanga ni mahali sahihi kwake.Akizungumza na Championi Jumamosi, Nsimbe alisema: “Siwezi kumkataza mchezaji kuondoka kama ameamua, lakini huyu ni mchezaji muhimu kwetu na ningependa abaki.
“Nitajitahidi kumshauri abaki lakini kama ataamua mwenyewe kuondoka, basi aende tu maana moyo wake utakuwa umependa kufanya hivyo. Naamini wapo wanaoweza kucheza nafasi yake,” alisema kocha huyo wa zamani wa KCCA ya Uganda.
Habari kutoka ndani ya Yanga zinasema uongozi unafanya jitihada zote kuhakikisha Kavumbagu anasajiliwa kwani ni chaguo la Kocha Hans van der Pluijm ambaye hana mshambuliaji wa uhakika katika kikosi chake.

Wednesday, May 6, 2015

NUSU FAINALI LIGI YA MABINGWA ULAYA JUVENTUS vs REAL MADRID LEO


Mghana Huyu Mpya Simba Noma Sana

Mshambuliaji wa Simba raia wa Ghana, Aboagye Gerson.
Wilbert Molandi na Sweetbert Lukonge
WAKATI mchakato wa usajili wa kimyakimya ukiendelea kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara, Simba jana ilimshusha mshambuliaji raia wa Ghana, Aboagye Gerson aliyekuwa anakipiga Klabu ya Zhako ya Iraq.
Ujio wa Mghana huyo ni mipango ya kukiboresha kikosi hicho katika kuelekea msimu ujao baada ya Kocha Mkuu wa Simba, Goran Kopunovic kutoa mapendekezo ya usajili wa mshambuliaji mmoja anayejua kazi yake inavyotakiwa.
Simba imekuwa ikikosa mshambuliaji mwenye makali tangu alipoondoka Amissi Tambwe mwanzoni mwa msimu huu huku Dan Sserunkuma aliyeziba pengo akishindwa kuwa hatari katika ufungaji.
Mghana huyo, anayecheza nafasi ya ushambuliaji namba tisa, alikuwa mmoja wa walioshiriki katika mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa ajili ya majaribio kabla ya kupewa mkataba.
Straika huyo alionyesha uwezo mkubwa katika kumiliki na kupiga pasi katika muda wa saa moja na nusu alizopewa mazoezini hapo.
Alipiga mashuti makali kiasi cha kusababisha mashabiki waliojitokezauwanjanihapo kujiuliza mchezaji huyo ametokea wapi.Aidha, alionyesha uwezo mkubwa wa kumiliki mpira na kumpa tabu beki Mganda, Juko Murshid aliyekuwa akimkaba.
Alipoulizwa Kopunovic juu ya mchezaji huyo alisema: “Nimemuona kwa muda mfupi, ni ngumu kuzungumzia uwezo wake, lakini kwa kifupi tu bado ninahitaji muda wa kumuangalia.
“Siku mbili au tatu kwangu hazinitoshi kujua uwezo wake na kushawishi kutoa mapendekezo ya kumsajili, ninaomba muda zaidi, isitoshe kipindi hiki siyo kizuri kwangu kwa ajili ya kuangalia wachezaji wakati tukiwa tupo kwenye ligi,” alisema Kopunovic.Mshambuliaji huyo naye alisema: “Hiki siyo kipindi changu cha kuzungumza, kwa kifupi nimekuja kwa ajili ya majaribio.”

Yanga Wasema Hatumbebi Mtu

Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro.
Khadija Mngwai, na Said Ally
YANGA inatarajia kushuka dimbani leo Jumatano kuvaana na Azam FC katika mchezo ambao itakabidhiwa kombe na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara kwenye mchezo ambao unaweza kutoa taswira ya juu ya timu itakayoshika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu Bara kati ya Azam au Simba, lakini tamko la Jangwani ni kuwa ‘habebwi mtu’.
Ikiwa Yanga itaifunga Azam itakuwa ni faida kwa Simba kwa kuwa itakuwa na matumaini ya kushika nafasi ya pili ili kuwakilisha nchi kimataifa, lakini ikiwa Yanga itafungwa basi hapo ndipo ndoto za Simba kushiriki Kombe la Shirikisho msimu ujao zitakuwa zimezimika rasmi.
Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro, amefunguka juu ya mchezo huo huku akiwapa masharti magumu Simba, pia ameeleza mambo mengine mbalimbali katika mkutano wake na waandishi wa habari jana katika makao makuu ya klabu hiyo jijini Dar.
Hatutambeba mtu
“Hatutaki watu watuingilie katika mchezo wetu wa leo, kwani ubingwa tumeuchukua sisi wenyewe, hivyo hatutaki kero. Watu wasitupangie jinsi ya kucheza hata kidogo, kwani sisi wenyewe ndiyo wenye maamuzi ya nini tufanye katika mchezo huu.
“Maandalizi yanaendelea vizuri, kumekuwa na maneno mengi kutoka kwa mashabiki mbalimbali kuwa tutawaachia Azam ili kuikomoa Simba.“Nataka watu wajue kuwa hatujakaa kuzungumza na klabu yoyote ile na wala hatufikirii kufanya hivyo kwa ajili ya kupanga matokeo. Hatutamsaidia mtu wala kumuonea mtu, tutapambana wenyewe kwani tulivyotwaa ubingwa ni kwa juhudi zetu binafsi, tusihusishwe kupanga matokeo.”
Niyonzima, Msuva hawaondoki
“Kumekuwa na maneno mengi kuhusiana na wachezaji wetu, Haruna Niyonzima na Simon Msuva kuwa huenda wakatua Simba msimu ujao, jambo hilo ni la uongo na hawatakwenda huko na wala Yanga haifikirii kusajili mchezaji yeyote kutoka Simba msimu ujao, hili ni pendekezo la uongozi uliopo madarakani kwa sasa.”
Aveva, Hans Poppe wavae jezi za Yanga
“Kama watani wetu wa Simba wanahitaji kusaidiwa basi na sisi katika mchezo wetu ni vema viongozi wao wa juu, Zacharia Hans Poppe na Evans Aveva wajitokeze uwanjani kesho (leo) kuja kutushangilia huku wakiwa wamevaa jezi za Yanga, wakifanya hivyo wanaweza kupata huruma yetu.”
Usajili Yanga
“Kwa upande wetu bado hatujapata pendekezo lolote kutoka kwa kocha kuhusiana na usajili na hatujui hadi sasa nani atabaki na nani ataondoka msimu ujao.“Tunasubiri pendekezo kutoka kwa kocha wetu, Hans van Der Pluijm ambaye atasema mchezaji gani anamhitaji. Hukumu ya wachezaji wote ambao watahitajika na wale wanaotakiwa kuondoka itabakia mikononi mwa kocha.”
Viongozi hakuna kusajili
“Kwa jinsi mikakati tuliyoipanga sasa hivi, hatuhitaji kiongozi yeyote kuingilia mipango ya usajili wetu kwa kuleta wachezaji wao kusajiliwa zaidi ya kocha pekee ambaye ndiye mwenye mamlaka ya kusajili wachezaji.”
Tatizo dola
“Kutokana na kupanda kwa dola katika viwango vya kubadilishia fedha, ilitulazimu bajeti yetu kuwa juu katika mchezo wetu dhidi ya Etoile du Sahel ambapo ‘ilitukosti’ zaidi ya shilingi milioni 96, tofauti na ilivyokuwa awali tulipocheza na BDF XI ya Zimbabwe.”
Yanga yaomba kombe lotelote
“Uongozi wa klabu upo mbioni kupeleka mapendekezo kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuanzisha mfumo wa kulibakiza kombe kwa timu husika mara baada ya kulitwaa na si kombe hilo kuzunguka kila mwaka katika timu zitakazoshinda.”

Mchezaji wa Yanga Aibiwa Gari Huku Akipambana Tunisia

Kipa wa Yanga, Ally Mustapha ‘Barthez’.
Wilbert Molandi,Dar es Salaam
WATU wanaodaiwa kuwa ni majambazi, wameiba gari la kipa wa Yanga, Ally Mustapha ‘Barthez’, aina ya Toyota Carina SI lenye namba za usajili T 224 CXR.
Akizungumza na Championi Jumatano, Barthez alisema kuwa gari hilo liliibiwa usiku wa kuamkia Ijumaa iliyopita wakati yeye akiwa safarini akielekea Tunisia kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Etoile du Sahel uliomalizika kwa Yanga kufungwa bao 1-0.
Barthez alisema kuwa, gari hilo liliibiwa kwenye maegesho ya magari eneo la Majumba Sita, Ukonga jijini Dar es Salaam. Akisimulia mkasa huo kwa masikitiko makubwa, Barthez alisema aliliacha gari hilo mikononi mwa mdogo wake hadi linakumbana na mkasa huo.
“Ninaishi Kitunda nilipojenga nyumba ninayoishi na familia yangu, mara nyingi ninaposafiri ninamuachia mdogo wangu Aziz Mustapha anayeishi Majumba Sita kwa ajili ya kulilinda.
“Kwa sababu kule kwangu ninapoishi vibaka wapo wengi na mara nyingi wamekuwa wakiruka ukuta na kuiba baadhi ya vitu vilivyopo kwenye gari. Wakati narejea nchini nikiwa kwenye Uwanja wa Ndege, ndiyo nikampigia simu mdogo wangu na kunipa taarifa za kuibiwa gari hilo. “Hivyo nikatumia usafiri mwingine kwenda Majumba Sita walipo wazazi wangu ndiyo wakanipa taarifa hizo kuwa gari liliibiwa usiku wa kuamkia Ijumaa iliyopita.
“Nilipohoji vipi mlinzi alikuwa wapi, mdogo wangu akanijibu kuwa alipokwenda asubuhi alikuta gari na mlinzi wote hawapo na ndiyo akaenda kuripoti kituo cha polisi, wakati anafika hapo akakutana na watu wengine watatu waliofika kuripoti kuibiwa gari kwenye maegesho hayo ya gari.
“Polisi wanaendelea na upelelezi kwa ajili ya kuchunguza wizi huo wa magari manne yaliyoibiwa,” alisema Barthez. Mshambuliaji wa Yanga, Simon Msuva anayemiliki gari aina ya Altezza, naye alitoa masikitiko yake. “Kwa kweli nimesikitika sana, nimempa pole Barthez kutokana na tukio hilo baya.
Mimi mwenyewe kila nikisafiri nimekuwa namuachia mzee gari anakuwa nalo maana pale nyumbani kuna watu wengi na ulinzi upo.“Nachofanya ni kujaza mafuta ya kutosha na mzee anaendelea na misele yake. Siku nikirudi nalichukua,” alisema Msuva.
Kwa upande wa Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, alisema: “Kweli inauma sana, kwa kweli wamefanya kitu kibaya sana.“Mimi nimekuwa makini sana, mara nyingi nikisafiri naliacha nyumbani Kigamboni ambako kuna ndugu zangu na familia yangu.”