YANGA inatarajia kushuka dimbani leo Jumatano kuvaana na Azam FC katika mchezo ambao itakabidhiwa kombe na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara kwenye mchezo ambao unaweza kutoa taswira ya juu ya timu itakayoshika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu Bara kati ya Azam au Simba, lakini tamko la Jangwani ni kuwa ‘habebwi mtu’.
Ikiwa Yanga itaifunga Azam itakuwa ni faida kwa Simba kwa kuwa itakuwa na matumaini ya kushika nafasi ya pili ili kuwakilisha nchi kimataifa, lakini ikiwa Yanga itafungwa basi hapo ndipo ndoto za Simba kushiriki Kombe la Shirikisho msimu ujao zitakuwa zimezimika rasmi.
Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro, amefunguka juu ya mchezo huo huku akiwapa masharti magumu Simba, pia ameeleza mambo mengine mbalimbali katika mkutano wake na waandishi wa habari jana katika makao makuu ya klabu hiyo jijini Dar.
Hatutambeba mtu
“Hatutaki watu watuingilie katika mchezo wetu wa leo, kwani ubingwa tumeuchukua sisi wenyewe, hivyo hatutaki kero. Watu wasitupangie jinsi ya kucheza hata kidogo, kwani sisi wenyewe ndiyo wenye maamuzi ya nini tufanye katika mchezo huu.
“Maandalizi yanaendelea vizuri, kumekuwa na maneno mengi kutoka kwa mashabiki mbalimbali kuwa tutawaachia Azam ili kuikomoa Simba.“Nataka watu wajue kuwa hatujakaa kuzungumza na klabu yoyote ile na wala hatufikirii kufanya hivyo kwa ajili ya kupanga matokeo. Hatutamsaidia mtu wala kumuonea mtu, tutapambana wenyewe kwani tulivyotwaa ubingwa ni kwa juhudi zetu binafsi, tusihusishwe kupanga matokeo.”
Niyonzima, Msuva hawaondoki
“Kumekuwa na maneno mengi kuhusiana na wachezaji wetu, Haruna Niyonzima na Simon Msuva kuwa huenda wakatua Simba msimu ujao, jambo hilo ni la uongo na hawatakwenda huko na wala Yanga haifikirii kusajili mchezaji yeyote kutoka Simba msimu ujao, hili ni pendekezo la uongozi uliopo madarakani kwa sasa.”
Aveva, Hans Poppe wavae jezi za Yanga
“Kama watani wetu wa Simba wanahitaji kusaidiwa basi na sisi katika mchezo wetu ni vema viongozi wao wa juu, Zacharia Hans Poppe na Evans Aveva wajitokeze uwanjani kesho (leo) kuja kutushangilia huku wakiwa wamevaa jezi za Yanga, wakifanya hivyo wanaweza kupata huruma yetu.”
Usajili Yanga
“Kwa upande wetu bado hatujapata pendekezo lolote kutoka kwa kocha kuhusiana na usajili na hatujui hadi sasa nani atabaki na nani ataondoka msimu ujao.“Tunasubiri pendekezo kutoka kwa kocha wetu, Hans van Der Pluijm ambaye atasema mchezaji gani anamhitaji. Hukumu ya wachezaji wote ambao watahitajika na wale wanaotakiwa kuondoka itabakia mikononi mwa kocha.”
Viongozi hakuna kusajili
“Kwa jinsi mikakati tuliyoipanga sasa hivi, hatuhitaji kiongozi yeyote kuingilia mipango ya usajili wetu kwa kuleta wachezaji wao kusajiliwa zaidi ya kocha pekee ambaye ndiye mwenye mamlaka ya kusajili wachezaji.”
Tatizo dola
“Kutokana na kupanda kwa dola katika viwango vya kubadilishia fedha, ilitulazimu bajeti yetu kuwa juu katika mchezo wetu dhidi ya Etoile du Sahel ambapo ‘ilitukosti’ zaidi ya shilingi milioni 96, tofauti na ilivyokuwa awali tulipocheza na BDF XI ya Zimbabwe.”
Yanga yaomba kombe lotelote
“Uongozi wa klabu upo mbioni kupeleka mapendekezo kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuanzisha mfumo wa kulibakiza kombe kwa timu husika mara baada ya kulitwaa na si kombe hilo kuzunguka kila mwaka katika timu zitakazoshinda.”


No comments:
Post a Comment